Prof Ndalichako awaonya waliopanga kufanya udanganyifu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wanafunzi wa darasa la saba kuepuka udanganyifu katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.
Wanafunzi hao wanafanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi Septemba 8 hadi 9 mwaka huu ikiwa ni awamu ya kwanza tangu utaratibu wa elimu bila malipo uanze nchini.
Profesa Ndalichako ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 6, 2021 baada ya kukagua ujenzi wa shule ya mfano inayojengwa katika kata ya Iyumbu jijini Dodoma.
Ujenzi wa shule hiyo uliofikia asilimia 60 unagharimu Sh17.1 bilioni na unatarajiwa kukamilika Februari mwaka 2022.
Profesa Ndalichako amesema maandalizi ya mitihani hiyo imekamilika na vifaa pamoja na mitihani imeshasambazwa kwenye vituo.
“Miaka miwili mitatu iliyopita kumeanza kuwa na vidalili dalili vya kuijaribu Serikali watu wamekuwa wakifanya udanganyifu katika mitihani. Naomba niwatadharishe kuwa Serikali iko imara na tutakuwa makini katika kuhakikisha mitihani inafanyika kwa kuzingatia taratibu,”amesema.
Amesema yeyote atakayeshulika na vitendo vya udanhanyifu Serikali itachukua hatua kwa mujibu wa taratibu.
“Niwatakie kila la kheri…hamna haja ya kuwa na wasiwasi na msikubali kuingizwa katika vitendo vya udanganyifu kwa sababu una madhara,”amesema.
Comments
Post a Comment