Wapenzi wa Simba Lindi wahaha kutafuta jezi mpya, wajipanga kikamilifu kushiriki Siku ya Simba
Na Ahmad Mmow, Lindi.
Vilio vya wanachama, washabiki na wapenzi wa timu ya soka ya Simba( Wenye nchi) vinasikika mjini Lindi pia. Baada ya jitihada za kupata jezi mpya za timu hiyo kugonga mwamba mara mbili.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba wa tawi la Mshikamano ambao ulifanyika jana mjini Lindi, katibu wa tawi hilo, Ibrahim Mwaya alisema kupata jezi mpya za Simba imekuwa ni kazi ngumu ambayo hawakuitarajia.
Mwaya ambae maelezo yake yaliungwa mkono na mtunza hazina wa tawi hilo, Omari Mswahili alisema licha ya kuwepo fedha za kununulia jezi hizo lakini changamoto ni kupata. Kwani mahitaji ni makubwa.
Alisema licha ya kutuma fedha Dar-es-Salaam, lakini aliyetumiwa akanunue alikutana na ugumu uliosababisha fedha hizo ambazo zinatosha kununua jozi za jezi takribani 200 zilireshwa.
" Huyo mtu aliamua kurejesha, baada ya kukosa jezi kwenye maduka ya Vunjabei. Alikuta misururu mikubwa na mwisho akaahidiwa Jumatatu( leo) uhenda atapata,'' alisema Mwaya.
Katibu huyo wa tawi la Mshikamano alisema baada ya kukosa Dar-es-Salaam waliagiza Mbeya ambako pia kuna maduka ya Vunjabei. Ambako pia walishindwa kupata, baada ya kumbiwa jezi zilizopo zinauzwa kwa bei ya rejareja.
Mbali ya hilo la jezi lakini pia tawi hilo limepanga kushiriki kikamilifu siku ya Simba( Simba day). Kwamujibu wa mwenyekiti wa tawi hilo, Salum Fundi.
Fundi alisema maandalizi kabambe yanafanyika ili kuahakikisha wiki ya Simba day washabiki, wanachama na wapenzi wanashiriki shughuli za kijamii na kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wenye uhitaji.
Fundi pia alisema wanachama na wapenzi wa tawi hilo wanatarajia kwenda kwa wingi jijini Dar-es-Salaam ili kushiriki siku ya kilele ya wiki hiyo.
" Usafiri tayari upo. Kwenda na kurudi Dar ni shilingi 30,000 tu na michango inaendelea kutolewa ili tukaishangilie na kuiona timu yetu pendwa na wachezaji wapya," alisema Fundi.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa washabiki , wanachama na wapenzi kuwasilisha michango kwa wakati.

Comments
Post a Comment